Jumapili 21 Desemba 2025 - 10:00
Wanaodai Uongo Kwamba ni Manaibu wa Imamu

Hawza/ Bila shaka, kila itikadi inayokaribia zaidi ukweli na kupenya kwenye nyoyo za watu, hupelekea zaidi watu wenye tamaa kujitokeza wakitafuta manufaa machafu kupitia itikadi hiyo. Mafundisho ya Mahdawiyya pia, kwa sababu ya sifa zake za kipekee na mvuto wake mkubwa, na kwa kuwa daima yamepenya ndani kabisa ya nyoyo za umma, yamekuwa zaidi yakilengwa na watu wasiofaa kwa ajili ya kuyatumia vibaya na kuyageuza kwa maslahi yao binafsi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, mfululizo wa masomo ya Mahdawiyya kwa anuani isemayo “Kuielekea Jamii Bora”, kwa lengo la kusambaza mafundisho na maarifa yanayohusiana na Imam wa Zama, (ajt), yanaletwa kwenu wasomi kama ifuatavyi:

Nafasi na athari kubwa ya “Mahdawiyya” na mafundisho yake kwa mtu binafsi na kwa jamii haifichiki kwa yeyote. Kwamba Waislamu—hasa Mashia—wana imani thabiti katika msingi huu muhimu na wanauhesabu kuwa miongoni mwa itikadi zao za kina na za msingi, ni jambo lililo wazi na lisilopingika.

Bila shaka, kila itikadi iliyo ya kina zaidi, iliyo karibu zaidi na ukweli, na iliyojikita katika nyoyo, huwavutia zaidi watu wenye tamaa wanaotafuta manufaa yasiyo halali kupitia hiyo.

Mafundisho ya Mahdawiyya, kwa sababu ya sifa zake za kipekee na mvuto wake mkubwa, na kwa kuwa daima yamepenya ndani ya nyoyo za wanadamu, yamekuwa zaidi yakilengwa na watu waliopotoka kwa matumizi mabaya na yasiyo sahihi. Historia pana ya upotovu uliojitokeza katika uwanja huu—hasa makundi potofu katika Mahdawiyya yanayorejea katika karne za mwanzo za Uislamu—ni ushahidi wazi wa dai hili. Kuchunguza upotovu huu na sababu za kuibuka kwake kunaweza kuwa na mchango muhimu katika kuzuia kuanguka tena katika makosa haya.

Dai la uongo la uwakilishi: mwanzo wa upotovu mkubwa

Kwa kuwa baada ya kuuawa kishahidi Imam Hasan al-Askari alayhi s-salam na kuanza kwa Ghayba Ndogo, mawasiliano ya moja kwa moja kati ya watu na kiongozi maasumu yalikatika, “mabalozi maalumu” walianza juhudi pana kwa namna ya kipekee ili kuwaongoza watu. Walizuia kusambaratika wafuasi wa madhehebu ya Ahlul-Bayt alayhim s-salam na wakachukua uongozi wa Mashia mikononi mwao.

Katika mazingira haya, watu fulani wenye imani dhaifu na fikra potofu, kwa ajili ya kufikia malengo mbalimbali, waliongipa kuwa ni wawakilishi wa Imam aliyeghaibu.

Baadhi ya sababu za madai haya ya uongo zinaweza kuorodheshwa kama ifuatavyo:

1. Udhaifu wa imani

Miongoni mwa sababu muhimu za madai haya yasiyo sahihi ni udhaifu wa imani ya kidini; kwa sababu wale walio na imani thabiti kamwe hawapotoki na kwenda kinyume na matakwa ya kiongozi maasumu — hasa katika kuwafuata mabalozi wake.

Mmoja wa watu waliozusha madai yasiyo sahihi kutokana na udhaifu wa imani alikuwa ni Shalmaghani. Alikuwa ni miongoni mwa wafuasi wa Imam Hasan al-Askari alayhi s-salam na miongoni mwa wanazuoni, waandishi na wapokezi wa hadithi katika zama zake huko Baghdad. Alikuwa na vitabu vingi ambavyo vilijaa maneno ya Ahlul-Bayt alayhim s-salam.
(Rijal al-Najashi, j. 2, uk. 239)

Alipokengeuka na kurejea nyuma, na akabadilika katika fikra, itikadi na mwenendo, alianza kufanya mabadiliko katika riwaya; aliongeza alichotaka na kupunguza alichotaka. Najashi amebainisha upotovu huu katika kitabu chake cha Rijal.
(Shaykh Tusi, al-Fihrist, uk. 305; Rijal al-Najashi, j. 2, uk. 294)

2. Tamaa katika mali za Imam

Katika kipindi cha Ghaiba Ndogo, baadhi ya watu, ili wasikabidhi mali za Imam wa Zama alayhi s-salam kwa wakala na mwakilishi wake halali, walidai uwakilishi.

Abu Tahir Muhammad bin Ali bin Bilal ni miongoni mwa watu waliodai ubabiya kwa lengo la kujilimbikizia mali. Mwanzoni alikuwa mtu anayeaminika mbele ya Imam Hasan al-Askari alayhi s-salam na alinukuu riwaya kutoka kwake; lakini polepole, kwa kufuata matamanio ya nafsi, alikengeuka na akalaumiwa na Ahlul-Bayt wa wahyi. Alidai kuwa yeye ni wakala wa Imam Mahdi Mola aharakishe faraja yake.

Alikanusha uwakilishi wa naibu wa pili wa Imam na akafanya khiyana katika mali zilizokuwa zimekusanywa kwake ili zimfikie Imam Mahdi ajaAllah Ta‘ala farajahu sharif.
(Kitab al-Ghayba, uk. 400)

3. Kutafuta umaarufu

Kutafuta umaarufu pia ni miongoni mwa sababu muhimu sana za kuibuka kwa imani za kishirikina na madhehebu bandia. Tamaa ya kujitukuza na kujionesha ni miongoni mwa sifa mbaya za kimaadili ambazo humvuta mtu kuelekea katika matendo hatari.

4. Motisha za kisiasa

Sababu nyingine ya kuibuka kwa wadai wa ubabiya ni motisha za kisiasa. Maadui, wakati mwingine moja kwa moja na wakati mwingine kwa njia isiyo ya moja kwa moja — kwa lengo la kudhoofisha imani ya Mashia na kuwaingiza katika mifarakano —huwachochea baadhi ya watu kudai ubabiya.

Katika njia hii, walilea baadhi ya watu kwa misingi ya matakwa yao, wakawaamuru kudai ubabiya, na wakawasaidia kwa kila aina ya nyenzo. Mfano wake ni “Sayyid Ali Muhammad Shirazi (1235 H – 1266 H), mwanzilishi wa dini ya Babiya, anayejulikana miongoni mwa wafuasi wake kama Babiya.”

Utafiti huu unaendelea…

Imenukuliwa kutoka katika kitabu “Darsnameh Mahdawiyya; kilichoandikwa na Khodamorad Soleymiyan”, huku ikifanyiwa mabadiliko kiasi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha